Serikali imesema haina mamlaka ya kuzipangia benki za biashara viwango vya riba za mikopo, ikieleza kuwa gharama hizo huamuliwa kwa kuzingatia hali ya soko, mfumuko wa bei, vihatarishi vya mikopo na gharama za uendeshaji wa benki.
Kauli hiyo imetolewa leo bungeni na Naibu Waziri wa Fedha Laurent Luswetula, wakati akijibu swali la Mbunge wa Mpanda Mjini, Haidary Sumry, aliyetaka kujua iwapo Serikali haioni haja ya kupunguza riba za mikopo ya biashara ili kuwawezesha wafanyabiashara kulipa madeni yao kwa wakati.
Naibu Waziri huyo, amesema Serikali haiingilii moja kwa moja upangaji wa viwango vya riba katika benki za biashara zinazofanya shughuli zake nchini, kwa kuwa viwango hivyo huamuliwa kwa kuzingatia misingi ya soko.
Amesema miongoni mwa mambo yanayoathiri viwango vya riba ni mfumuko wa bei, vihatarishi vya mikopo kutolipwa, gharama za uendeshaji wa benki na kiwango cha faida kinacholengwa na benki husika.
Hata hivyo, amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kisera na kiusimamizi zinazolenga kuwezesha wananchi kupata mikopo kwa gharama nafuu zaidi.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kutekeleza sera ya fedha inayolenga kudhibiti mfumuko wa bei, ambao ni moja ya viashiria muhimu vinavyotumika katika kukokotoa na kuamua viwango vya riba za mikopo.
Amesema katika kufanikisha azma hiyo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendelea kufanya marekebisho katika kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) kulingana na mwelekeo wa uchumi.
Amefafanua kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha mfumuko wa bei unabaki ndani ya wigo unaokubalika, huku ikiendelea kuwepo kwa ukwasi wa kutosha katika uchumi ili kuchochea upatikanaji wa mikopo kwa gharama nafuu.
Aidha, amesema Serikali pia imeanzisha Price Comparator System, mfumo unaolenga kuongeza uwazi kuhusu viwango vya riba na gharama nyingine zinazotozwa na taasisi mbalimbali za kifedha.
Amesema mfumo huo utawawezesha wakopaji kulinganisha gharama za mikopo kutoka taasisi mbalimbali na kufanya maamuzi sahihi kabla ya kuchukua mikopo.
โMfumo huo unaongeza uwazi kuhusu viwango vya riba na gharama zinazotozwa na taasisi mbalimbali za kifedha, na hivyo kuwasaidia wakopaji kufanya maamuzi sahihi kuhusu huduma za mikopo wanazozihitaji,โ amesema.
Vile vile, amesema mfumo huo unalenga kuchochea ushindani miongoni mwa benki za biashara, hali ambayo inaweza kuchangia kupunguza gharama za mikopo kwa wananchi.
Pia, amesema Serikali inaendelea kuhimiza benki na taasisi za fedha kutumia Credit Reference Bureau, kanzidata inayohifadhi taarifa za historia ya ukopaji na ulipaji wa madeni ya wakopaji.
Amesema matumizi ya taarifa hizo yanasaidia benki kutathmini uwezo na historia ya mkopaji na kupunguza hofu kuhusu uwezekano wa mikopo kutolipwa.
Kwa mujibu wa Waziri, hali hiyo inaweza kusaidia kupunguza gharama za tathmini ya mikopo na hatimaye kuchangia upatikanaji wa mikopo yenye gharama nafuu zaidi.
Serikali imesisitiza kuwa pamoja na kutopanga moja kwa moja riba za benki, inaendelea kutumia sera za fedha, kuongeza ushindani na uwazi katika sekta ya kifedha pamoja na kuboresha mifumo ya taarifa za wakopaji, hatua zinazolenga kupunguza gharama ya mikopo kwa wananchi na wafanyabiashara.
