Wakulima mkoani Morogoro wameiomba serikali iwapatie mikopo wakati wa kilimo ili kuepukana na mikopo umiza inayotolewa na watu binafsi yenye riba kubwa wanayoirejesha wakati wa mavuno na kushindwa kunufaika na mfumo wa stakabadhi ghalani.

Mkulima mmoja wa Kakao kutoka wilayani Mvomero mkoani Morogoro Samwel Joseph amesema hayo leo kwenye maonesho ya Nane nane kanda ya Mashariki.

Amesema AMCOS nyingi  hazijawezeshwa mitaji ya kuwasaidia wakulima kama mikopo kutoka serikalini na kusababisha kujiingiza kwenye mikopo umiza na hivyo kujikuta wakiweka dhamana shamba zima na kukosa kuona faida ya kilimo.

"Utakuta mkulima amekopa fedha za kuandalia shamba na tatizo huja pale akikopa hela nyingi hulazimu shamba lake kuwekwa bondi na Kakao yake kukosa fursa ya soko zuri iliyoandaliwa na serikali kupitia stakabadhi ghalani," amesema Joseph.

Pia Joseph ameishukuru serikali kwa kuweka mfumo wa stakabadhi ghalani unaowasaidia wakulima kuona tija ya kilimo na kuingiza kipato kinachowasaidia kukidhi mahitaji ya nyumbani.

Joseph Alfonce ni mkulima wa ufuta na mbaaza katika kijiji cha Sesenga kata ya Mngazi wilayani Morogoro ambaye anasema mfumo wa stakabadhi ghalani umewasaidia wakulima kuwa na bei moja ya mazao na kuepuka kudhulumiwa na walanguzi ambao walikuwa wakipanga wenyewe bei za bila kumjali mkulima.

Meneja wa chama cha ushirika cha wakulima mkoani Morogoro (MOFACU) Andrew Bellah amesema kwa sasa serikali inafanya utaratibu ili kuanzisha Saccos za wakulima kwenye vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS) na kuwakopeshwa wakulima kukabiliana na maandalizi ya mashamba kwa ajili ya kilimo.