Na Calvin Minja – DCC


Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Mhe. Nurdin Bilal “Shetta”, ameahidi kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Bajeti ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ili kuhakikisha mipango yote iliyoidhinishwa inatekelezwa kwa ufanisi, uwazi na kuleta matokeo chanya kwa wananchi.


Mhe. Bilal ametoa kauli hiyo leo, Julai 30, 2026, katika Ukumbi wa Karimjee wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani kilichopokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa shughuli za Kamati mbalimbali za Halmashauri kwa robo ya nne ya mwaka wa fedha 2025/2026. Kamati hizo, zinazoongozwa na madiwani, ziliwasilisha taarifa za utekelezaji wa majukumu yao kwa kipindi husika.


Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Bilal amesema mafanikio yaliyopatikana katika mwaka wa fedha 2025/2026 yanapaswa kuwa msingi wa kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa Bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027.


Tutahakikisha bajeti hii inatekelezwa kwa ufanisi, uwazi na uwajibikaji ili wananchi wa Jiji la Dar es Salaam wapate huduma bora na maendeleo yaliyokusudiwa,” amesema.


Aidha, Mstahiki Meya amewapongeza Madiwani, kamati mbalimbali za Halmashauri, Mkurugenzi wa Jiji, Menejimenti pamoja na watumishi wote kwa ushirikiano wanaoendelea kuuonesha katika kutekeleza majukumu ya Halmashauri na kumuunga mkono Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.


Amesema ushirikiano huo umeendelea kuwa chachu ya mafanikio ya Halmashauri katika kutekeleza vipaumbele vya Serikali na kuimarisha ustawi wa wananchi wa Jiji la Dar es Salaam.