Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeendelea kuimarisha juhudi za kupanua wigo wa hifadhi ya jamii nchini kwa kuwahamasisha wananchi waliojiajiri kujiunga na Hifadhi Skimu, huku ikiwahimiza waajiri wenye malimbikizo ya michango kunufaika na msamaha wa tozo uliotolewa na mfuko huo.

Akizungumza baada ya kutembelea banda la mfuko huo jana katika maonesho ya Sabasaba, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, alisema ameridhishwa na mwitikio wa wananchi pamoja na huduma zinazotolewa na mfuko, hususan elimu kuhusu hifadhi ya jamii, usajili wa wanachama wapya na huduma za kidijitali.

Mshomba alisema banda la NSSF limeendelea kuwa jukwaa muhimu la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu nafasi ya hifadhi ya jamii katika kuboresha ustawi wa maisha, kupunguza umaskini, kuimarisha nguvu kazi na kuongeza uzalishaji katika uchumi wa taifa.

Kupitia Hifadhi Skimu, alisema: “wananchi waliojiajiri wanaweza kujiunga na mfuko huo kwa hiari na kuchangia kwa viwango vinavyolingana na uwezo wao.”

Alieleza kuwa kiwango cha chini ni shilingi 30,000 kwa mwezi kinachomwezesha mwanachama kupata huduma za matibabu, huku mchango wa Sh 52,200 ukimpa mwanachama huduma za matibabu yeye mwenyewe, mwenza wake na watoto wasiozidi wanne.

“Wanachama wa skimu hii pia hunufaika na mafao ya uzazi, ulemavu, pensheni ya uzee na urithi, akibainisha kuwa mfumo huo unaruhusu michango kufanyika hata kila siku ilimradi ifikie kiwango cha mwezi,” alisema.

Waliojiajiri wahimizwa kujiunga na Hifadhi Skimu
Mshomba alisema mafanikio hayo yametokana na maboresho ya chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambayo yameongeza ushiriki wa wananchi waliojiajiri katika mfumo rasmi wa hifadhi ya jamii.

Katika huduma za kidijitali, alisema NSSF imeboresha mifumo yake inayowezesha wanachama na waajiri kujihudumia popote kupitia NSSF Portal bila kufika ofisini, hatua iliyorahisisha upatikanaji wa huduma kwa wakati.

“Pia NSSF imetoa msamaha wa tozo kwa waajiri wenye madeni ya michango kuanzia Juni hadi Desemba 2026, ili kuwapa fursa ya kulipa madeni ya msingi na kupunguza mzigo wa tozo,” alisema.

Alisema waajiri watakaolipa madeni yao ya msingi kuanzia Juni hadi Agosti 31, 2026 watanufaika na msamaha wa asilimia 100 ya tozo, mradi waendelee kulipa michango ya sasa kwa wakati hadi Januari 2027.

Waliojiajiri wahimizwa kujiunga na Hifadhi Skimu
Aidha, alieleza kuwa wataakaoanza kulipa kati ya Septemba mosi na Oktoba 31 watanufaika na msamaha wa asilimia 75, huku watakaoanza kulipa kati ya Novemba mosi na Desemba 31 wakinufaika na msamaha wa asilimia 50.

Aliwataka waajiri kutumia fursa hiyo kuongeza tija katika uzalishaji badala ya kuelekeza rasilimali katika kulipa tozo, huku akisisitiza umuhimu wa kuwasilisha michango kwa wakati ili kulinda haki za wafanyakazi.

Pia aliwahimiza waajiriwa kufuatilia michango yao na kutoa taarifa NSSF endapo michango yao haiwasilishwi kwa mujibu wa sheria.