Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ipo katika hatua za mwisho za kuanzisha huduma ya utoaji mikopo kupitia simu za mkononi ikiwa ni jitihada za kupunguza utegemezi wa mikopo isiyo rasmi maarufu kama kausha damu.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Frank Nyabundege, ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 30,2026 jijini Dodoma, ambapo amesema benki hiyo inakamilisha uunganishaji wa mifumo yake na kampuni za simu ili huduma hiyo ianze kutolewa.
Amesema mikopo ya kausha damu imekuwa ikiwafilisi wakulima kutokana na riba kubwa na kwamba mpango huo unalenga kuwapa wakulima fursa ya kupata mikopo midogo kwa haraka kupitia simu, badala ya kukimbilia wakopeshaji binafsi wanaotoza riba kubwa na masharti magumu ya urejeshaji.
"Kwa sasa tuko katika hatua za mwisho za kuwezesha mifumo yetu na mitandao ya simu ili mwananchi, badala ya kwenda kukopa kausha damu, aweze kukopa benki kupitia simu yake," alisema.
Akizungumzia maendeleo ya TADB, Nyabundege amesema benki hiyo imejipanga kuongeza kasi ya uwekezaji katika sekta ya kilimo,mifugo na uvuvi kupitia utoaji wa mitaji,matumizi ya teknolojia na ushirikiano na wadau ili kuchochea uchumi wa Taifa na kufanikisha DIRA ya Maendeleo 2050.
Amesema mtaji wa benki hiyo umeongezeka kutoka Sh bilioni 60 ilipoanzishwa mwaka 2015 hadi Sh bilioni 793 kutokana na uwekezaji wa Serikali na mikopo yenye masharti nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo.
Ukuaji huo umeiwezesha benki kuongeza mikopo iliyotolewa kutoka Sh bilioni 294 mwaka 2021 hadi Sh trilioni 1.55 mwaka 2025, huku zaidi ya asilimia 80 ya fedha hizo zikitolewa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita.
