Naibu Kamishna wa Idara ya Upelelezi wa Kodi, Felisiana Nkane, amekutana na watumishi wapya wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wanaoendelea na mafunzo elekezi katika Chuo cha Kodi jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu majukumu ya idara hiyo na mbinu za kubaini na kudhibiti ukwepaji wa kodi.

Nkane amesema Idara ya Upelelezi wa Kodi ina jukumu la kulinda mapato ya Serikali kwa kupambana na uhalifu wa kiuchumi, hususan ukwepaji kodi, kupitia ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa za kiintelijensia.

Amesema mafunzo hayo yatawawezesha watumishi hao kutekeleza majukumu yao kwa weledi watakapopangiwa vituo vya kazi, huku akiwataka kuzingatia taratibu za ukusanyaji na uchakataji wa taarifa hadi kukamilisha uchunguzi.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, uadilifu na kujituma, akieleza kuwa misingi hiyo ni muhimu katika kufikia malengo ya TRA.

Nkane pia amewataka watumishi hao kushirikiana kwa karibu na wadau pamoja na watoa taarifa, akisema ushirikiano huo ni muhimu katika kuimarisha mapambano dhidi ya ukwepaji kodi na kuongeza mapato ya Serikali.