Shirika la Fedha Duniani (IMF) limeridhishwa na utendaji kazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuahidi kuendeleza ushirikiano katika kuwezesha biashara, uwekezaji na utawala wa kodi.

Vilevile, IMF imeipongeza TRA kwa kuendelea kufanya usimamizi mzuri wa kodi na kuwezesha biashara na uwekezaji nchini.

Pongezi hizo zilitolewa jana katika makao makuu ya TRA jijini Dar es Salaam wakati uongozi wa IMF ulipofanya mazungumzo kuhusu masuala ya kodi na manajimenti ya TRA iliyoongozwa na Kamishana Mkuu, Yusuph Mwenda.

Akizungumza katika ziara hiyo, Kiongozi wa msafara wa IMF, Thabo Letjama amesema IMF inaridhishwa na utendaji kazi wa TRA na kuwapongeza kwa kuendelea kufanya usimamizi mzuri wa kodi na kuwezesha biashara na uwekezaji nchini.

"Mamajimenti ya IMF imeeidhishwa na namna TRA inavyofanya kazi hususani ya ushirikiano na uhusiano mzuri na wafanyabiashara katika kukusanya kodi. IMF itaendelea kuahirikana na TRA katika masuala yote," amesema Letjama.

Aidha ameipongeza TRA kwa kuwa karibu na walipakodi na kuahidi kuendeleza uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo baina ya TRA na IMF kwenye kuwezesha biashara, uwekezaji na utawala wa kodi.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA, Mwenda amesema TRA imeimarisha na kuboresha zaidi uhusiano mzuri na walipakodi kote nchini hali ambayo imeongeza kwa kiasi kikubwa uhiari katika kulipa kodi na kuongeza makusanyo ya Kodi.

Amesema TRA pia imekuwa ikifanya juhudi za kuongeza wigo wa kodi kwa kusajili walipakodi wapya huku ikiwezesha biashara na shughuli nyingine za uchumi sambamba na kuendelea kuimarisha mifumo ya kodi ya kidigitali kupitia IDRAS kwa kodi za ndani na TANCIS kwa upande wa Forodha.

Mwenda amesema TRA itaendelea kushirikiana na IMF na kuboresha usimamizi katika utawala wa kodi kwa wakati marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa walipakodi wenye vigezo.

Katika kikao cha tathmini ya utendaji kazi kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kilichofanyika hivi karibuni TRA imejiwekea lengo la kukusanya Sh.trilioni 41.830 katika mwaka wa fedha 2026/27.

Kamishna Mkuu wa TRA,ย  Yusuph Mwenda, alisema mikakati waliyoweka katika kikao hicho itawawezesha kukamilisha na kuvuka lengo la kukusanya Sh. trilioni 41.830.