MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umewataka wazazi, walezi, waajiri na watu binafsi kuhakikisha wanajiunga na mfuko huo, kwa kuwakatia watoto wao bima, ili kujikinga na gharama kubwa za matibabu na kuwawezesha kupata huduma bora za afya kwa wakati.
Ofisa Matekelezo wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Tanga, Macrina Clemens, amesema hayo wakati wa utoaji elimu kuhusu Bima ya Afya, iliyokwenda sambamba na upimaji afya, usajili wa wanachama wa Vifurushi iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Ushirika wa Makorora, jijini Tanga.
Macrina amesema afya njema ni msingi wa maendeleo ya familia na taifa, hivyo kujiunga na Bima ya Afya ni hatua muhimu ya kujikinga na gharama zisizotarajiwa za matibabu pia kuwapa wazazi utulivu wa akili watoto, wanapougua kwa kuwa wanakuwa na uhakika wa matibabu.
Macrina amesisitiza wanafunzi wanaosoma shuleni wanaweza kupata Bima ya Afya kupitia shule zao kwa gharama ya Sh. 50,400 kwa mwaka mzima wa masomo, vilevile alisema watoto ambao bado hawajaanza shule wanaweza pia kujiunga kupitia vifurushi vinavyotolewa na NHIF.

