umla ya vikundi 28 vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika Manispaa ya Iringa vimefanikiwa kupata mkopo wa asilimia 10 wenye thamani ya Sh milioni 402 kwa kipindi cha robo ya nne ya mwaka wa fedha 2025/2026 (Aprili hadi Juni).
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi hundi pamoja na bajaji na bodaboda kwa vikundi vilivyonufaika, Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Zaina Mlawa, amesema fedha hizo zimegawanywa kwa makundi mbalimbali, ambapo watu wenye ulemavu wamepata zaidi ya Sh milioni 96, vijana zaidi ya Sh milioni 153 na wanawake zaidi ya Sh milioni 152.
Mlawa amesema vikundi vilivyonufaika vilipitia mchakato wa tathmini na upembuzi yakinifu kuanzia ngazi ya kata, manispaa hadi menejimenti kabla ya kupitishwa kupata mikopo hiyo.
"Vikundi vyote vilivyopata mikopo vilifanyiwa tathmini ya kina kuanzia ngazi ya kata hadi menejimenti ya manispaa ili kuhakikisha vinastahili kunufaika na fedha hizi," amesema Mlawa.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Mwatumu Dossi, amesema vikundi 49 havikufanikiwa kupata mkopo baada ya kubainika kuwa baadhi yake vilitoa taarifa zisizo sahihi, ikiwemo kuwasilisha biashara ambazo sio zao.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sita, amesema maafisa maendeleo ya jamii wanapaswa kuendelea kutoa elimu ya ujasiriamali kwa vikundi ambavyo havikufanikiwa ili viweze kukidhi vigezo na kunufaika katika awamu zijazo.
"Maafisa maendeleo ya jamii waendelee kuwajengea uwezo vikundi ambavyo havikupata mikopo ili wakati ujao viwe na sifa za kunufaika," amesema Sita.
Pia amesema licha ya mikopo hiyo kutokuwa na riba, wanufaika wana wajibu wa kuirejesha kwa wakati ili kutoa nafasi kwa vikundi vingine kupata huduma hiyo.
"Mikopo hii haina riba, lakini ni lazima irejeshwe kwa wakati. Msibadilishe miradi mliyoiombea fedha, zitumieni vizuri ili biashara zenu zikue na wengine wapate fursa ya kukopa," amesema.
Aidha, amesema nidhamu katika usimamizi na urejeshaji wa mikopo midogo ndiyo msingi wa wafanyabiashara kupata mikopo mikubwa zaidi siku zijazo.
Kwa upande wa wanufaika, mwakilishi wa kundi la watu wenye ulemavu, Anifa Luhala, amesema wanaishukuru Serikali kwa kuwawezesha na kuahidi kuwa wataitumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa pamoja na kuirejesha kwa wakati.
"Tunashukuru Serikali kwa kutuamini na kutupatia mkopo huu. Tumejipanga kuutumia vizuri na kuurejesha kwa wakati uliopangwa," amesema Luhala.
Naye Mbunge wa Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, amesema watendaji wa Manispaa ya Iringa wanapaswa kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ili wananchi wengi zaidi wanufaike na programu za uwezeshaji wa kiuchumi.


