Meneja wa TIRA Kanda ya Kaskazini, Dkt. Emmanuel Lupilya akizungumza kwenye kikao hicho jijini Arusha

Afisa Bima wa TIRA Kanda ya Kaskazini, Goodluck Massawe akizungumza kwenye kikao hicho jijini Arusha .

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya African Time, Melkizedeck Festo akizungumza kwenye kikao hicho jijini Arusha
……..
Na Happy Lazaro, Arusha
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Kanda ya Kaskazini imewakutanisha wamiliki wa gereji kanda ya kaskazini na kuweza kuweka mipango na utaratibu utakaorahisisha uchukuaji, tathmini na ukarabati wa magari yaliyopata ajali, huku ikisisitiza ushirikiano kati ya magereji, kampuni za bima na mamlaka.
Meneja wa TIRA Kanda ya Kaskazini, Dkt. Emmanuel Lupilya ameyasema hayo jijijni Arusha katika kikao chake na wamiliki hao ambapo amesema kuwa , katika utaratibu huo, gereji iliyo karibu na eneo ambalo ajali imetokea ndiyo itakayohusika kwanza kuchukua gari na kulipeleka kwa ajili ya kuanza mchakato wa tathmini.
Amesema tathmini ya uharibifu itafanywa kwa ushirikiano kati ya gereji, wataalamu waliopo na mthamini kutoka kampuni ya bima husika, pamoja na wataalamu wengine pale itakapoonekana kuna umuhimu wa kuwashirikisha.
Amesema utaratibu huo utasaidia kuhakikisha gharama za matengenezo zinakubalika na pande zote kabla ya kuanza kwa kazi za ukarabati, hatua ambayo inalenga kupunguza migogoro na malalamiko yanayoweza kujitokeza.
Dkt. Lupilya amesema kuwa , mteja hatanyimwa haki ya kuchagua gereji anayopendelea, lakini mchakato wa awali utaanzia katika eneo la ajali na gari kupelekwa kwenye gereji inayohusika kwa ajili ya tathmini.
“Hatukatai mteja kuchagua sehemu ya gereji kwenda, lakini pointi ya kwanza ni kwamba mahali pale ambapo ajali imetokea ndipo mchakato utaanzia,” amesema.
Ameongeza kuwa endapo gereji ya kwanza itaona haiwezi kuhudumia gari kutokana na kiwango cha uharibifu, gari hilo linaweza kupelekwa kwenye gereji nyingine yenye uwezo unaohitajika.
Amesema endapo gereji kadhaa zitashindwa kulirekebisha gari hilo kutokana na kiwango cha uharibifu, suala hilo linaweza kuhitaji kuamuliwa kama gari limeharibika kiasi cha kuwa “write-off”, au mteja na kampuni ya bima kukubaliana hatua inayofuata.
Dkt. Lupilya amesema TIRA pia inatarajia kukutana na kampuni za bima na waandishi wa bima (underwriters) ili kujadili kwa pamoja utaratibu huo na kuhakikisha pande zote zinaelewa na kutekeleza mfumo mmoja.
Amesema moja ya maeneo muhimu yatakayojadiliwa ni namna ya kudhibiti udanganyifu wa bima na viashiria mbalimbali vya udanganyifu, huku kampuni za bima zikitakiwa kuwa sehemu ya juhudi hizo pamoja na magereji na TIRA.
Aidha, amesema TIRA inalenga kuondoa changamoto inayoweza kujitokeza pale kampuni ya bima inapomlipa mteja moja kwa moja badala ya kulipa gereji iliyofanya ukarabati, jambo ambalo linaweza kusababisha migogoro kati ya mteja, gereji, kampuni ya bima na mamlaka ya usimamizi.
Amesema mfumo huo mpya ukitekelezwa kwa ushirikiano utasaidia kuongeza ufanisi, kupunguza malalamiko na kujenga uaminifu zaidi katika sekta ya bima, huku Kanda ya Kaskazini ikitarajiwa kuwa miongoni mwa maeneo yatakayonufaika zaidi na fursa hizo.
“Yajayo yanafurahisha sana na yajayo yatakuwa ni makubwa sana katika Kanda hii ya Kaskazini,” amesema Dkt. Lupilya.
Hata hivyo ametumia fursa hiyo kuzitaka gereji zote kanda ya kaskazini zinazohusika na ukarabati na utengenezaji wa vyombo vya moto kusajiliwa na kupata ithibati kutoka mamlaka hiyo ili kurahisisha usimamizi na utatuzi wa changamoto zinazoweza kujitokeza kati yao na kampuni za bima.
Naye Afisa Bima wa TIRA Kanda ya Kaskazini, Goodluck Massawe amesema kikao hicho kililenga kuwakumbusha watengeneza na warekebishaji wa vyombo vya moto kuhusu majukumu yao pamoja na namna wanavyopaswa kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia miongozo iliyowekwa na mamlaka.
Massawe amesema TIRA imesisitiza kwa wadau hao kuhakikisha wanazingatia maelekezo yote yaliyowekwa na mamlaka, hususani yale yanayohusu miongozo ya utoaji wa huduma za ukarabati wa magari yaliyokatwa bima.
Kwa upande wao washiriki wa kikao hicho ambao ni wamiliki wa gereji mbalimbali kanda ya kaskazini, wamesema kuwa ,usajili wa gereji ni muhimu kwa kuwa unaziwezesha kampuni za bima kufanya kazi na gereji husika kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
Akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya African Time, Melkizedeck Festo, amesema usajili wa gereji ni muhimu kwa kuwa unaziwezesha kampuni za bima kufanya kazi na gereji husika kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Arusha Art Limited ,Hemal Sachdev inayojihusisha na maswala ya gereji pamoja na uwakala wa magari mbalimbali nchini, amepongeza kikao cha mafunzo kuhusu masuala ya bima na usajili wa gereji, akisema kimewasaidia kupata uelewa mpana kuhusu taratibu na maendeleo ya sekta hiyo.
Amesema mafunzo hayo yamewapa fursa ya kujifunza mambo mbalimbali ambayo awali hayakuwa yakifahamika kwa wamiliki wengi wa gereji, ikiwemo taratibu za kusajili gereji, kampuni pamoja na namna ya kuendesha shughuli hizo kwa kufuata mifumo na taratibu zilizowekwa.
