Na Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma

Serikali imewekeza katika miradi mbalimbali yenye thamani ya takribani Shilingi bilioni 66.7 katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), kwa lengo la kuongeza uwezo wa uchunguzi na matibabu ya saratani, kupunguza muda wa kusubiri huduma na kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi.Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 17,2026 jijini Dodoma, kuhusu Utekelezaji wa Mwaka wa Fedha 2025/26 na Mwelekeo wa Mwaka wa Fedha 2026/27 wa ORCI , MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dkt. Diwani Msemo, amesema uwekezaji huo umehusisha ujenzi wa miundombinu na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa, ikiwemo PET Scan, ELEKTA Harmony, Linear Accelerator, mashine mbili za Cobalt, SPECT na Mammography.

Aidha, Sh. bilioni 11 zimeelekezwa katika ujenzi wa Kituo cha Saratani Mbeya, ambacho kimefikia asilimia 57 ya utekelezaji na kinatarajiwa kukamilika Januari 2027 na kuanza kutoa huduma Julai 2027, huku kikilenga kuwahudumia wananchi wa Nyanda za Juu Kusini pamoja na nchi jirani za Zambia, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

 Ameongeza Kuwa ORCIinaendelea na ujenzi wa Multipurpose Oncology Building wenye thamani ya takribani Sh. bilioni 5.9, ambao umefikia asilimia 65 na unatarajiwa kukamilika Desemba 2026, ukiwa na wodi za wagonjwa, maeneo ya tiba ya kemikali, kliniki, maabara, famasia na ofisi za wataalamu.

Amesema katika tiba ya mionzi, Serikali imewekeza takribani Sh. bilioni 7.9 katika Linear Accelerator ambayo tayari imeanza kutoa huduma, huku mashine mbili za Cobalt zenye thamani ya takribani Sh. bilioni 4.3 zikiwa katika hatua ya asilimia 95 ya usimikaji na zikitarajiwa kuanza kutumika Septemba 2026.

Ameongeza kuwa ORCI imefungwa PET Scan yenye thamani ya Sh. bilioni 18.2, ELEKTA Harmony yenye thamani ya Sh. bilioni 8.3 na SPECT yenye thamani ya Sh. bilioni 1.5, huku mashine mbili za Mammography zenye thamani ya takribani Sh. bilioni 1.1 zikiwa katika hatua za usimikaji kwa ajili ya kuimarisha uchunguzi wa saratani ya matiti.

Huku akibainisha Kuwa uwekezaji huo umeongeza uwezo wa kugundua saratani katika hatua za awali na kubaini hatua ambayo ugonjwa umefikia, huku lengo likiwa kupunguza muda wa kusubiri tiba ya mionzi hadi wastani wa takribani wiki mbili baada ya mgonjwa kukamilisha uchunguzi.

Amesema uwekezaji umeenda sambamba na kuimarisha rasilimali watu, ambapo watumishi 66 wamehudhuria kozi mbalimbali, madaktari bingwa saba wa upasuaji wamesharejea kutoka masomoni na wengine wanne wanaendelea na masomo, huku huduma za upasuaji mkubwa zikitarajiwa kuanza Oktoba 2026.

Akizungumzia huduma za uchunguzi wa mapema, amesema ORCI kupitia kampeni ya Tiba Mkoba imefika katika mikoa 15 na kutoa huduma za uchunguzi wa awali wa saratani kwa zaidi ya watu 200,000, huku maandalizi ya kuanzisha vituo vipya vya saratani Mtwara, Kigoma na Arusha yakiendelea.

Amesema uwekezaji huo unalenga kuongeza uwezo wa ORCI kuhudumia wagonjwa wengi zaidi kutoka ndani na nje ya nchi, kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi na kuimarisha Tanzania kuwa kituo cha huduma za saratani katika ukanda wa Afrika, huku akiwataka wananchi kupima afya mara kwa mara ili saratani igundulike mapema.