Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza kuanza kutumika kwa Kanuni za Fedha za Kigeni (Marekebisho) za Mwaka 2026, zinazowaruhusu wawekezaji wote wasio wakazi kuwekeza katika dhamana za Serikali za muda mfupi na muda mrefu zinazotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hatua hiyo inalenga kupanua ushiriki katika soko la dhamana za Serikali, kuendeleza masoko ya fedha nchini na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha uwekezaji katika ukanda.

Kwa mujibu wa taarifa ya BoT, kanuni hizo zimetungwa chini ya Sheria ya Fedha za Kigeni, Sura ya 271, kupitia Tangazo la Serikali Na. 206 la mwaka 2026 lililochapishwa katika Gazeti la Serikali la Julai 17, 2026.

Kabla ya marekebisho hayo, ushiriki katika soko la dhamana za Serikali uliruhusiwa kwa wakazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Watanzania wanaoishi nje ya nchi pekee.

Kupitia marekebisho hayo, wawekezaji wote wasio wakazi sasa watakuwa na fursa ya kuwekeza katika dhamana za Serikali kupitia mawakala wa uwekezaji, kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa katika Kanuni za Fedha za Kigeni (Marekebisho) za Mwaka 2026 pamoja na sheria nyingine husika na taratibu za kiutendaji zinazotolewa na Benki Kuu ya Tanzania.

BoT imesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha maendeleo ya masoko ya fedha nchini, kuongeza ushindani katika soko la dhamana za Serikali na kuvutia mitaji kutoka masoko ya kimataifa.

Kanuni za Fedha za Kigeni (Marekebisho) za Mwaka 2026 zinapatikana kupitia tovuti rasmi ya Benki Kuu ya Tanzania kwa ajili ya wadau wanaotaka kupata maelezo zaidi kuhusu masharti na taratibu za utekelezaji wa kanuni hizo.