Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umewataka wananchi kujiunga na bima ya afya ili kuepuka kuuza mali na kutumia akiba waliyoitunza pindi wanapougua na kukabiliwa na gharama za matibabu.

Meneja Masoko na Huduma kwa Wateja wa NHIF, Angela Mziray, ameyasema hayo wakati akizungumzia umuhimu wa bima katika maonyesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, akisema gharama za matibabu zinaweza kuathiri uchumi wa familia endapo mwananchi hana bima ya afya.

Amesema baadhi ya wananchi hulazimika kuuza mali, mashamba na rasilimali nyingine ili kugharamia matibabu wanapopatwa na ugonjwa ambao unagharimu fedha nyingi wakati ambao hawakujiandaa kifedha.

“Ni muhimu wananchi kujidunduliza kidogo kidogo na kuchangia bima ya afya ili ugonjwa unapokuja kwao au familia zao wawe na uhakika wa kupata huduma za matibabu,” amesema.

Mziray amesema wananchi wanapaswa kuona bima ya afya kama kinga ya kifedha, kwa kuwa inawawezesha kuchangia gharama za matibabu kabla ya kuugua badala ya kusubiri kutumia fedha nyingi wakati wanapohitaji huduma.

Amesema NHIF inatumia maonyesho ya Nanenane kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuwa na bima ya afya, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.

Kwa mujibu wa Mziray, huduma zinazotolewa kupitia bima hiyo zinapatikana katika vituo vya kutolea huduma za afya vya Serikali, binafsi na vya mashirika ya dini vilivyosajiliwa na mfuko na kusema matumizi ya bima ya afya yanaweza kusaidia familia kulinda rasilimali zao na kuepuka kuelekeza fedha zilizotengwa kwa shughuli za maendeleo kwenye gharama za matibabu zisizotarajiwa.