Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea kutoa elimu kuhusu mabadiliko ya Sheria na Taratibu za Forodha yaliyotokana na Sheria ya Fedha ya mwaka 2026, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuwawezesha wadau wa forodha kuelewa na kutekeleza ipasavyo mabadiliko hayo.

Mafunzo hayo yamefanyika katika Kituo cha Pamoja cha Forodha cha Sirari (Sirari OSBP), ambapo washiriki pia wamehimizwa kushiriki kikamilifu katika juhudi za kuzuia na kutokomeza vitendo vya magendo vinavyoathiri uchumi wa Taifa.

Elimu hiyo ilitolewa na Afisa Mfawidhi wa Forodha Mkoa wa Dodoma, Hassan Minga, kwa kushirikiana na Afisa Mkuu wa Forodha kutoka Makao Makuu ya Forodha, Allan Maduhu.

Wakizungumza na wadau wa forodha, maofisa hao walisisitiza umuhimu wa kuzingatia mabadiliko yote ya sheria na taratibu mpya, wakieleza kuwa utekelezaji sahihi wa sheria za forodha unachangia kurahisisha biashara halali, kuongeza ufanisi wa huduma za forodha na kuziba mianya inayoweza kutumiwa kufanikisha vitendo vya magendo.

Aidha, waliwahimiza wadau kuendelea kushirikiana na TRA katika kulinda mapato ya Serikali kwa kufuata sheria na kutoa taarifa kuhusu vitendo vinavyohatarisha mfumo wa biashara halali.

Washiriki wa mafunzo walipata fursa ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kuhusu maeneo mbalimbali ya mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2026, hatua iliyowawezesha kuongeza uelewa na kujiandaa kutekeleza kwa usahihi matakwa ya sheria na taratibu mpya za forodha.

Baadhi ya washiriki walisema mafunzo hayo yamewajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, huku yakiongeza uelewa kuhusu wajibu wao katika kushirikiana na TRA kupambana na biashara haramu, magendo na vitendo vya ukwepaji wa kodi.

TRA imeendelea kusisitiza kuwa ushirikiano kati ya Mamlaka na wadau wa forodha ni msingi muhimu katika kuhakikisha biashara zinafanyika kwa kuzingatia sheria, kudhibiti magendo, kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kujenga mazingira ya ushindani wa haki kwa wafanyabiashara wanaozingatia sheria.