Serikali imeweka mikakati mipya ya kupunguza matumizi ya fedha taslimu na kuziba mianya inayoweza kutumika katika utakatishaji wa fedha haramu kwa kuanzisha utaratibu wa lazima wa matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali katika miamala mbalimbali nchini.

Hatua hiyo imewekwa kupitia marekebisho ya Sheria ya Miamala ya Kielektroniki, Sura ya 442 pamoja na kutungwa kwa Amri inayobainisha miamala inayopaswa kufanyika kwa njia za kielektroniki, ambapo mtu anayefanya au kupokea malipo katika miamala hiyo anatakiwa kutumia njia rasmi za kidijitali.

Akizungumza jinini Dodoma,wakati wa mafunzo kwa Mawakili wa Serikali kuhusu mabadiliko yaliyotokana na Sheria ya Fedha ya mwaka 2026, Mkurugenzi Msaidizi wa Divisheni ya Uandishi wa Sheria kutoka Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD), Chresencia Mathayo amesema mfumo huo utasaidia kuongeza uwazi na kurahisisha ufuatiliaji wa miamala nchini.

Amesema matumizi ya njia za kidijitali yataongeza usalama wa fedha na kusaidia kuziba mianya inayoweza kutumika katika utakatishaji wa fedha haramu, ukwepaji wa kodi na vitendo vingine vya uhalifu wa kifedha.

โ€œMatumizi ya njia za kidijitali katika miamala yanarahisisha ufuatiliaji wa malipo, yanaongeza usalama wa fedha na yatasaidia kuziba mianya inayoweza kutumika katika utakatishaji wa fedha haramu,โ€ amesema Chresencia.

Amesema njia zinazotambulika kuwa za kidijitali ni pamoja na fedha kwa simu, uhamisho wa fedha kupitia benki, kadi za malipo, mashine za malipo (POS), huduma za benki kwa njia ya mtandao au simu pamoja na mifumo ya malipo ya Serikali.

Amesema baadhi ya miamala ambayo inapaswa kufanyika kwa njia za kidijitali ni pamoja na malipo ya ada za shule, nauli za vyombo mbalimbali vya usafiri, huduma za hoteli na migahawa, shughuli za utalii, pamoja na malipo ya ununuzi na upangishaji wa majengo, mashamba na viwanja.

Aidha, amesema Kanuni za Utoaji wa Leseni za Biashara zimefanyiwa marekebisho ambapo wafanyabiashara wanatakiwa kuambatanisha uthibitisho wa matumizi ya mfumo wa malipo ya kidijitali kama Lipa Namba au TANQR wakati wa kuomba au kuhuisha leseni zao.

Amesema hatua hiyo imelenga kuhakikisha miamala ya biashara inapitia katika mifumo rasmi ya kifedha, huku ikipunguza gharama na hatari zinazotokana na matumizi ya fedha taslimu kama vile wizi na upotevu wa fedha. Mabadiliko hayo yameanza kutumika rasmi Julai Mosi, 2026.