Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umewatambua wanachama 7,881 wanaotarajiwa kustaafu katika mwaka wa fedha 2026/27, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha wanapata mafao yao kwa wakati kupitia kaulimbiu ya ‘Tunalipa Jana’.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Uendeshaji wa PSSSF, Hajj Khamisi, alipozungumza katika banda la Mfuko kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere.

Amesema Mfuko ulianza maandalizi mapema kwa kushirikiana na waajiri ili kuhakikisha mchakato wa ulipaji mafao unakamilika bila ucheleweshaji.

Khamisi amewashukuru waajiri kwa kuendelea kuwasilisha madai ya watumishi kwa wakati, akisema ushirikiano huo unarahisisha Mfuko kuyachakata madai na kuwezesha wastaafu kupata mafao yao kwa wakati.

“Hii itasaidia kutekeleza kaulimbiu yetu ya ‘Tunalipa Jana’ na kuwaletea tabasamu wastaafu wetu,” ameongeza.

Akizungumzia mchango wa teknolojia katika kuboresha huduma, Mkurugenzi wa TEHAMA wa PSSSF, Eric Kato, amesema mifumo ya kidijitali ya Mfuko imeboreshwa kwa kiwango kikubwa, jambo lililorahisisha utoaji wa huduma kwa wanachama.

Amesema kupitia mifumo hiyo, wanachama wanaweza kuwasilisha madai yao wakiwa popote walipo bila kulazimika kusafiri, hatua inayookoa muda na gharama.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Fedha wa PSSSF, Ally Yakuti, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwezesha Mfuko kwa kuwasilisha michango ya wanachama kwa wakati.

Amesema hali hiyo imeuwezesha Mfuko kutekeleza wajibu wake wa kulipa mafao ya mkupuo na pensheni za kila mwezi bila kuchelewesha wanachama wanaostaafu.

Baadhi ya wastaafu wanaopokea pensheni kupitia PSSSF walithibitisha kupata malipo yao kwa wakati, wakisema mfumo wa Mfuko umeendelea kuimarika.

Naye Said Mohammed amesema wakati mwingine pensheni huingia mapema kuliko ilivyozoeleka.